Yanga Yalalamika Kuhusu Adhabu na Makosa ya Waamuzi Ligi Kuu
2026-03-08 - 04:38
Klabu ya Yanga Machi 3, 2026 imetoa malalamiko makali dhidi ya Kamati ya Saa 72 na Bodi ya Ligi ikihusisha adhabu, makosa ya waamuzi katika mechi mbalimbali za Ligi Tanzania Bara. Tofauti za Adhabu kwa Wachezaji: Yanga imeitaka Bodi ya Ligi kutoa ufafanuzi kuhusu adhabu iliyotolewa kwa mchezaji Selemani Mwalimu. Msimu huu, wachezaji watano walifungiwa mechi 5 kwa kosa linalofanana na Mwalimu, lakini yeye amefungiwa mechi 3 pekee. Klabu inaomba Bodi iweke bayana kwanini Kanuni ya 41:5(5.2) ilitumika kwa Mwalimu huku wachezaji wengine wakitumia Kanuni ya 41:21. Kuchelewa kwa Hukumu: Yanga imeuliza kwanini Kamati ya Saa 72 ilichelewa kukutana kufanya mapitio na kutoa hukumu, ikilinganishwa na mechi zingine ambapo hukumu zilitolewa kwa wakati. Klabu inaomba ufafanuzi wa sababu ya kucheleweshwa na changamoto zilizokuwapo. Adhabu Tofauti kwa Waamuzi: Klabu imelaani hukumu zilizotolewa kwa waamuzi wasaidizi 1 & 2 kwenye mechi ya Yanga SC dhidi ya Simba , kwa kosa la kushindwa kutafsiri sheria namba 11 (Offside). Ingawa wote walikosea sawa, mmoja alifungiwa miezi 6 na mwingine miezi 3. Yanga SC inataka kuelewa kigezo gani kilitumiwa kuchanganua adhabu tofauti. Goli Halali na Mamlaka ya Kamati: Klabu inakosoa kauli zilizotolewa kuhusu goli lililopewa Simba SC, ikisema sheria za FIFA zinabainisha kuwa goli halali ni lile tu linaloruhusiwa na mwamuzi wa kati, na hakuna kamati au kanuni inayoweza kuhalalisha goli lisiloruhusiwa. Kauli ya kwamba Simba “wamenyimwa goli halali” imesababisha taharuki kwa umma. Kutokukaa Makini kwa Kamati: Yanga pia imeitaka Bodi kutoa ufafanuzi kuhusu matukio ya mechi dhidi ya JKT, ambapo mwamuzi Glory Tesha alizuia nafasi mbili wazi za Yanga kufunga kwa madai ya kuotea, huku marejeo ya video yakionyesha kuwa wachezaji hawakuwa katika eneo la kuotea. Hadi sasa, kamati haijachukua hatua dhidi ya waamuzi hao. Yanga imesisitiza kuwa wanachama wa klabu wana haki ya kupata taarifa za wazi. Klabu imesema itawahabarisha wanachama kuhusu majibu kutoka Bodi ya Ligi, na kama majibu hayatatolewa, wanachama wataarifiwa kuwa Bodi haijatoa ufafanuzi.