Waziri Mkuu Kuanza Ziara Ya Kikazi Mkoani Arusha Februari 22, 2026
2026-02-21 - 12:07
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi mkoani Arusha kuanzia Februari 22 hadi 24, 2026, ambapo atatembelea na kukagua miradi sita yenye thamani ya shilingi bilioni 194.2 katika Wilaya za Arumeru, Longido na Arusha. Akizungumza Februari 21, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amesema siku ya kwanza ya ziara hiyo Waziri Mkuu ataweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa bweni la kisasa la Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Sayansi cha Nelson Mandela, kukagua upanuzi wa miundombinu ya Hospitali ya Oltrumet na kuzungumza na wananchi eneo la Ngaramtoni. Siku ya pili, Februari 23, atakuwa Wilaya ya Longido ambako atatembelea na kupokea taarifa ya mradi mkubwa wa maji Kata ya Sinya, kuzindua upanuzi wa Shule ya Sekondari Sinya hadi kufikia Kidato cha Tano na Sita, pamoja na kutembelea Kituo cha Huduma za Pamoja (One Stop Border Post) Namanga kabla ya kuzungumza na wananchi katika viwanja vya Shule ya Msingi Namanga. Kwa siku ya mwisho, Waziri Mkuu atatembelea Wilaya ya Arusha ambapo atakagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi eneo la Bondeni City, kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Soko la Kilombero na baadaye kuhutubia mkutano wa hadhara katika eneo hilo.