Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba Akagua Mradi wa Maji – Korogwe, Tanga
2026-02-16 - 10:30
WAZIRI MKUU Dkt Mwigulu Nchemba amekagua Mradi wa Maji wa Miji 28 unaoendelea kujengwa wilayani Korogwe mkoani Tanga kwa thamani ya sh. bilioni 171. Akizungumza na viongozi na wananchi waliofika kwenye eneo la tukio katika kijiji cha Mswaha Darajani, kata ya Mswaha Jumamosi, Februari 14, 2026, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na akasisitiza kuwa wananchi wanaoishi Mswaha ambalo ni jirani kabisa na eneo la mradi, wapewe kipaumbele cha kupata maji pindi utakapokamilka. Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi ya siku tano, amesema kuwa uwekezaji mkubwa umefanyika maeneo yote nchini kwa dhamiria ya kumaliza changamoto ya huduma ya maji kwa Watanzania wote. “Leo tunakuja kuuona mradi ambao hata kwa kuungalia tu unafurahisha, ni mradi wenye hadhi ya kiongozi anayejali mambo ya maendeleo. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameweka fedha hapa ili zisaidie wananchi wa Muheza, Handeni, Korogwe na Pangani,” amesema. “Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Rais anayejali maendeleo ya wananchi wake, na haya siyo maneno tu! Ninyi mnaona shughuli zinavyoendelea. Huu ni mradi wenye hadhi ya nchi inayoendelea, mradi wa aina hii siyo wa kutatua matatizo tu, bali unaipa hadhi nchi, ni mradi unaojali utu wa kila mwana Tanga, Muheza, Korogwe na Pangani,” amesisitiza Waziri Mkuu. Mapema, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema kuwa Wizara ya Maji inaendelea kutekeleza mkakati wa Gridi ya Taifa ya Maji ambapo kwa sasa Tanzania ina jumla ya mita za ujazo bilioni 126 za maji ambayo yatatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi. “Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitupa maelekezo kwamba Wizara ya Maji tutumie utajiri wa vyanzo vya maji vilivyopo Tanzania kumaliza changamoto ya maji kwa Watanzania. Alisema hataki kuona mwanamke wa Kitanzania akihangaika kutafuta maji ndipo akaanzisha kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani.”