Waziri Mkuu Asisitiza Amani, Maadili Na Ushirikiano Na Taasisi Za Dini – (Picha +Video)
2026-03-15 - 11:27
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za dini nchini katika kulinda amani, kuimarisha maadili na kuchochea maendeleo ya Taifa. Dkt. Mwigulu amesema hayo leo Jumapili (Machi 15, 2026) wakati akitoa salamu katika Ibada iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mpanda Mjini, Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, iliyoongozwa na Askofu Imani Ahobokile Chibona. Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za dini katika kujenga Taifa lenye hofu ya Mungu, upendo, haki na uwajibikaji. “Nimekuja pia na salamu za upendo kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye anatambua mchango mkubwa wa taasisi za dini katika kudumisha amani, maadili mema na mshikamano wa kitaifa,” amesema. Waziri Mkuu amesema taasisi za dini zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi, hususan katika sekta za elimu, afya na malezi ya jamii. Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Katavi ikiwemo miradi ya maji, barabara na nishati kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi. Akizungumzia sekta ya maji, Dkt. Mwigulu amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 ambapo jana aliweka jiwe la msingi la mradi wa kusambaza maji kutoka Bwawa la Milala unaotarajiwa kuzalisha lita milioni 12 za maji kwa siku na kuhudumia wakazi wa Manispaa ya Mpanda. Katika sekta ya miundombinu, amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara ya Mpanda – Tabora yenye urefu wa kilometa 352 kwa kiwango cha lami ambayo imekuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi katika mkoa huo. Aidha, amesema ujenzi wa barabara ya Mpanda – Uvinza – Kanyani unaendelea ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 15.7, huku ujenzi wa barabara ya Kagwira – Karema nao ukiendelea kwa lengo la kufungua fursa za kiuchumi katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.