Waziri Mkuu Afanya Royal Tour Arusha National Park
2026-01-31 - 15:39
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, leo Januari 31, 2026 amefanya ziara maalum maarufu kama “Royal Tour” katika Hifadhi ya Taifa Arusha (Arusha National Park), ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuitangaza sekta ya utalii na uhifadhi nchini. Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alipata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo, huku akipata maelezo kutoka kwa viongozi wa hifadhi kuhusu jitihada zinazoendelea za kulinda rasilimali za asili na kuongeza mchango wa utalii katika uchumi wa taifa. Aidha, Waziri Mkuu alikutana na kusalimiana na Braydon Bent Page, shabiki mkubwa wa klabu ya Manchester City, ambaye yupo nchini kwa ajili ya kutembelea vivutio vya utalii. Kukutana kwao kulionyesha mvuto wa utalii wa Tanzania kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani. Ziara hiyo ya Waziri Mkuu ni sehemu ya maandalizi kuelekea Tuzo za Utalii na Uhifadhi za Serengeti (Serengeti Tourism & Conservation Awards) zitakazofanyika jioni ya leo, ambapo Waziri Mkuu anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kupitia tuzo hizo, Serikali inalenga kuwatambua na kuwapongeza wadau wa sekta ya utalii na uhifadhi kwa mchango wao mkubwa katika kukuza utalii endelevu na kulinda rasilimali za asili za taifa.