Waziri Mkuu Aagiza Uchunguzi wa Mfumo Wa Upatikanaji wa Dawa Hospitalini
2026-03-15 - 13:57
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza kufanyika kwa uchunguzi kuhusu mfumo wa upatikanaji wa dawa katika hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Ametoa agizo hilo leo Jumapili (Machi 15, 2026) alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Nsimbo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Songambele mkoani Katavi, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo. Amesema Serikali imekuwa ikipeleka fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa katika hospitali na vituo vya afya, lakini bado baadhi ya wananchi wanapofika kutafuta huduma wanaelekezwa kwenda kununua dawa katika maduka binafsi nje ya hospitali. “Takwimu zinaonesha tuna utoshelevu wa dawa lakini mwananchi akienda hospitalini anaelekezwa mtaani kwenda kununua dawa. Huu mchezo haukubaliki. Duka la mtaani linapata wapi dawa ambayo Serikali haiwezi ikapata?” amesema. Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu amesema ni muhimu kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini namna fedha za ununuzi wa dawa zinavyotumika pamoja na mfumo wa upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya. Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu ameonya tabia ya baadhi ya viongozi kuuza ardhi ya vijiji kwa njia zisizo halali na kusababisha migogoro ya ardhi katika jamii. “Hata tukigombana ardhi haiongezeki. Binadamu tunaongezeka lakini ardhi haiongezeki. Hata tukipigana ardhi haiongezeki, kwa hiyo tuepuke kuchukiana kwa misingi hiyo,” amesema. Amesema Serikali haitavumilia vitendo vya utapeli wa ardhi vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wasiowaadilifu. “Watu wa aina hii wakishagundulika wasidunde mtaani lazima wafike kwenye mkono wa sheria. Wanataka kuvunja undugu wetu kwa tamaa na ubinafsi,” amesema. Kadhalika, Waziri Mkuu ameonya wakandarasi wanaolipwa fedha za miradi ya Serikali lakini wanashindwa kuwalipa mafundi na wakandarasi wadogo waliotekeleza kazi hizo. “Mkandarasi anapewa kazi anaajiri mafundi, anatoa subcontract kwa wengine, yeye analipwa fedha yote ya mradi lakini hawalipi wale waliofanya kazi. Watu wa aina hiyo wasakwe popote pale walipo na wasiwe huru mpaka wawalipe watu ambao wameshafanya kazi,” amesema. Amesema vitendo hivyo vinawanyima haki wananchi waliotekeleza kazi kwa uaminifu na vinaweza kuifanya jamii kuilaumu Serikali wakati fedha za miradi tayari zimeshalipwa kwa wakandarasi. “Hii kuchukua fedha Serikali imeshalipa halafu wananchi wetu ambao wamefanya kazi hawajalipwa ni kuwasababishia umaskini watu ambao wamefanya kazi kwa uaminifu,” amesema. Katika mkutano huo, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo sekta za afya, elimu na miundombinu. Amesema katika kipindi cha miaka minne iliyopita Serikali imejenga hospitali za wilaya 119, vituo vya afya 649 pamoja na zahanati zaidi ya 2,700 nchini kote kwa lengo la kuboresha huduma za afya kwa wananchi. Aidha, amesema Serikali imejenga zaidi ya shule za sekondari 1,300 pamoja na shule za ufundi zaidi ya 103 ili kuwawezesha vijana kupata elimu na ujuzi unaowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.