Watu Wawili Wafariki Katika Ajali ya Ndege Kugonga Gari la Uokoaji
2026-03-23 - 08:34
Ajali mbaya imetokea katika Uwanja wa Ndege wa LaGuardia uliopo New York, baada ya ndege ya shirika la Air Canada kugongana na gari la uokoaji wakati wa kutua usiku wa manane. Kwa mujibu wa taarifa za awali, ndege hiyo iliyokuwa ikitoka Montreal ilitua majira ya saa 11:40 usiku, kabla ya kugonga gari la uokoaji la Mamlaka ya Bandari (Port Authority) lililokuwa kwenye njia ya kurukia na kutua (runway), likijibu tukio jingine la dharura. Mgongano huo ulisababisha vifo vya rubani na co-pilot, huku abiria na watu wengine kadhaa wakiripotiwa kujeruhiwa. Ndege hiyo ilionekana kupata uharibifu mkubwa katika sehemu ya mbele, ambapo pua ya ndege (nose) iliharibika na kuinama mbele baada ya tukio hilo. Taarifa zaidi zinaeleza kuwa ndege hiyo ilikuwa ikiendeshwa na kampuni ya Jazz Aviation kwa niaba ya Air Canada. Mara baada ya ajali hiyo kutokea, mamlaka za uwanja wa ndege zilianzisha taratibu za dharura, huku Polisi wa Port Authority pamoja na viongozi wa taasisi hiyo wakifika eneo la tukio. Mamlaka husika zimesema zinafanya kazi kwa karibu na mashirika ya ndege pamoja na vyombo vya serikali ya shirikisho kuchunguza chanzo cha ajali hiyo, huku zikiahidi kutoa taarifa zaidi kadri uchunguzi unavyoendelea. Ajali hiyo imeacha simanzi kubwa na maswali mengi kuhusu usalama wa shughuli za uwanja wa ndege, hasa katika mazingira ya dharura ambapo magari ya huduma huweza kuwepo kwenye maeneo ya kurukia na kutua.