Wasira Awatolea Uvivu Walioanza Mbio Za Urais Mwaka 2030 (Picha +Video)
2026-03-28 - 04:04
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amewaonya wanachama walioanza harakati za kusaka urais mwaka 2030 akisema muda wa kufanya hivyo bado haujawadia, na wanaoanza mapema wanakiuka kanuni, miongozo na taratibu za chama. Amesema kuanza mapema harakati za kusaka uongozi kabla ya wakati kunaweza kukigawa chama badala ya kukijenga, hivyo tabia hiyo inapaswa kukemewa. Wasira ametoa kauli hiyo leo Mjini Bunda, Mkoa wa Mara, alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la ofisi za CCM Wilaya ya Bunda ambazo zilichomwa moto wakati wa vurugu za Oktoba 29, 2025. Amesema ndani ya chama kuna kundi la wanachama ambao hawana kazi za msingi zaidi ya kujihusisha na makundi ya kisiasa. Kwa mujibu wake, kundi hilo limeanza kujipanga kwa kuunda safu kuanzia ngazi za kata, hali inayoweza kusababisha mgawanyiko kwa kuwa kila mmoja anataka kuwa na wafuasi wake badala ya kuimarisha umoja. Wasira alihoji uhalali wa baadhi ya watu kuanza kujitangaza mapema kuwania urais wa 2030, akisema hakuna anayeweza kujihakikishia uwepo wake hadi wakati huo. “Unazungumziaje urais wa 2030 leo, wakati hata hujui kama utakuwepo? Hiyo ni kama kumjaribu Mungu. Wakati huu tunapaswa kujikita kwenye kazi za kujenga chama na nchi,” alisisitiza. Aidha, alionya tabia ya baadhi ya watu kutumia fedha kushawishi wanachama maskini ili waungwe mkono, akieleza kuwa hali hiyo ni hatari na inaweza kuharibu maadili ya chama.