Wanachama 11 wa Genge la Ulaghai la Ming Wanyongwa China
2026-01-29 - 10:24
Serikali ya China imetekeleza adhabu ya kunyongwa ya wanachama 11 wa familia maarufu ya Ming, iliyokuwa ikiendesha mitandao mikubwa ya ulaghai na kamari haramu nchini Myanmar. Mahakama ya Mkoa wa Zhejiang iliwahukumu wanachama hao mwezi Septemba mwaka jana kwa makosa mazito ikiwemo mauaji, kuwazuia watu kinyume cha sheria, ulaghai wa kimtandao pamoja na kuendesha nyumba haramu za kamari. Familia ya Ming ilikuwa miongoni mwa koo chache zenye nguvu kubwa zilizotawala mji wa Laukkaing uliopo karibu na mpaka wa China, ambapo chini ya utawala wao, mji huo maskini uligeuzwa kuwa kitovu cha kasino, biashara ya ngono na uhalifu wa kifedha. Milki ya ulaghai ya familia hiyo iliporomoka mwaka 2023 baada ya wanachama wake kukamatwa na kukabidhiwa kwa China na makundi ya kijeshi ya kikabila yaliyouteka mji wa Laukkaing, katika muktadha wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea Myanmar. Kwa miaka mingi, mitandao ya ulaghai nchini Myanmar imewanasa maelfu ya raia wa China pamoja na watu kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Afrika, ambapo waathirika wengi walitekwa au kusafirishwa kwa nguvu hadi katika kambi hizo na kulazimishwa kufanya ulaghai wa kimtandao dhidi ya raia wa mataifa ya nje. Mwaka jana, hasira za umma nchini China ziliongezeka baada ya kusambaa taarifa za muigizaji mdogo aliyesafiri kwenda Thailand kwa kazi ya uigizaji lakini baadaye akatekwa na kulazimishwa kupelekwa kwenye kituo cha ulaghai nchini Myanmar. Kwa mujibu wa Mahakama Kuu ya China, genge la Ming lilipata zaidi ya yuan bilioni 10 (sawa na dola bilioni 1.4 za Marekani) kati ya mwaka 2015 na 2023. Mahakama ilitupilia mbali rufaa zao mwezi Novemba, ikieleza kuwa uhalifu wa genge hilo ulisababisha vifo vya raia 14 wa China na kujeruhi wengine wengi.