Video: Tani 9.93 Za Dawa Za Kulevya Zakamatwa, Watuhumiwa 151 Wanaswa
2026-03-04 - 13:08
Tani 9.93 za dawa za kulevya aina mbalimbali, Mwezi Januari na Februari 2026, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilikamata tani 9.93 za dawa za kulevya za aina mbalimbali, chupa 1,795 za dawa tiba zenye asili ya kulevya na kuteketeza ekari 87.5 za mashamba ya bangi. Katika operesheni hizo, magari sita na pikipiki 29 zilikamatwa pamoja na watuhumiwa 151. Kwa kushirikiana na maafisa wa Forodha Mutukula, Mamlaka ilikamata boksi 105 za Pethidine (chupa 1,045), boksi 31 za Morphine Sulphate (chupa 310) na boksi 44 za Fentanyl (chupa 440). Dawa hizo zilikutwa katika basi la kampuni ya SR Classic lenye namba 5673AB04 kutoka Congo, lililokuwa likiingia nchini kupitia kituo cha forodha Mutukula. Watuhumiwa saba walikamatwa kuhusika na tukio hilo. Dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya pethidine boksi 105 zenye chupa 1,045, Morphine Sulphate boksi 31 zenye chupa 310 na Fentanyl boksi 44 zenye chupa 440 Dawa za Pethidine, Morphine na Fentanyl ni opioids zinazotumika hospitalini kupunguza maumivu makali. Hata hivyo, zikichepushwa, husababisha uraibu na zinaweza kuleta madhara makubwa ikiwemo vifo. Nchini, dawa hizo zimedhibitiwa kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95 na Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura ya 219, ambapo uingizaji na usambazaji wa nakotiki unafanywa na MSD pekee. Katika operesheni nyingine, bangi aina ya skanka ilikamatwa kwa wingi. Dar es Salaam, mtuhumiwa mmoja alikamatwa na kilo 81.883 za skanka ndani ya lori la Scania lililobeba matunda, huku Chanika Buyuni watuhumiwa wawili wakikamatwa na kilo 488.64. Mbeya, watuhumiwa sita walikamatwa wakisafirisha jumla ya kilo zaidi ya 76 za skanka. Arusha, watu wawili walikamatwa na bunda 937 za mirungi zenye uzito wa kilo 363.45. Aidha, katika operesheni zilizofanyika mikoa mbalimbali, zilikamatwa tani 5.24 za bangi, tani 4.04 za mirungi na gramu 72 za heroin.