Video: Mwajuma na Mwanaye Wauawa na Kutupwa Kisimani
2026-03-29 - 16:54
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limefanikiwa kuwakamata watu wanane wanaotuhumiwa kuhusika na matukio matatu tofauti ya uhalifu yaliyotokea katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Machi 29, 2026, watuhumiwa hao wanahusishwa na tukio la kwanza la mauaji ya mwanamke mmoja pamoja na mtoto wake mchanga wa miezi minne. Tukio hilo lilitokea Machi 28, 2026 majira ya saa 9 alasiri, ambapo miili ya marehemu Mwjabu Shaban (30) na mtoto wake Mwantumu Abdala ilikutwa imetupwa ndani ya kisima cha maji katika Kitongoji cha Tawini, Kijiji cha Kisangasa, Wilaya ya Kilindi. Watuhumiwa wanaohusishwa na tukio hilo ni pamoja na Kilo Msami, Abdallah Ibrahim, Hamis Ayub na Bigfai Edward. Aidha, watu wengine wawili, Sharifu Mustafa maarufu Charada na Adamu Ramadhan Hassani maarufu Masozy, wanashikiliwa kwa tuhuma za kumjeruhi vibaya Yassin Amiri, fundi simu mkazi wa Makorora Jijini Tanga. Katika tukio lingine, Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa wawili, Shani Gugu wa Kange Jijini Tanga na Bakari Hamza wa Moshi mkoani Kilimanjaro, kwa tuhuma za kukutwa na noti bandia 16 zenye thamani ya shilingi 160,000. Inadaiwa walikuwa wakizitumia noti hizo kwa kuzichanganya na fedha halali ili kujipatia bidhaa na huduma. Pia, Polisi imetoa taarifa ya tukio la mlipuko wa petroli lililotokea Machi 28, 2026 majira ya saa 12:30 jioni katika Kijiji cha Bongi, Kata ya Sindeni Wilaya ya Handeni, ambapo mtoto aitwaye Nilham Ramadhani (8) alipoteza maisha huku wengine watatu wakijeruhiwa na wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini. Katika operesheni nyingine, Polisi imekamata pikipiki 11 zisizo na namba za usajili, na uchunguzi unaendelea kubaini uhalali wake pamoja na kuchukua hatua za kisheria. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linaendelea na uchunguzi wa matukio hayo na linatoa wito kwa wananchi kuzingatia sheria na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kudhibiti uhalifu.