TheTanzaniaTime

Video: Basi la Maning Nice Lagonga Lori Lindi, Laua Wawili

2026-02-07 - 12:58

Watu wawili wamefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa katika ajali ya basi la Kampuni ya Maning Nice lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, baada ya kugonga lori lililokuwa limeharibika eneo la Mtange, Manispaa ya Lindi. Ajali hiyo imetokea leo Jumamosi Februari 7, 2026, saa 12 asubuhi na kusababisha vifo vya watu hao wawili akiwamo mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu. Akizungumza na waandishi wa habari, muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, Yusuph Salim amesema hospitali hiyo imepokea miili miwili pamoja na majeruhi 12 majira ya saa 1:15 asubuhi. Amesema kati ya majeruhi hao, wawili wamepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi, huku 10 wakiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.

Share this post: