UNDP Na Uingereza Wakutanisha Viongozi Wa Vyuo Vikuu Kukuza Ubunifu Zanzibar
2026-03-05 - 17:18
Na Neema Adrian – GPL Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP Tanzania), kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Chuo cha Indian Institute of Technology Madras Zanzibar, limewakutanisha viongozi wa vyuo vikuu, watunga sera na wadau wa ubunifu kutoka Afrika Mashariki katika mpango maalum wa kubadilishana wataalamu wa kitaaluma. Lengo ni kuviwezesha vyuo vikuu kuwa injini za ubunifu na ujasiriamali, badala ya kubaki kuwa vituo vya kuzalisha maarifa pekee. Mpango huo unalenga kuziba pengo lililopo kati ya tafiti na biashara, baada ya kubainika kuwa uvumbuzi mwingi unaishia maabara bila kuingia sokoni kama biashara endelevu. Kupitia kaulimbiu “Vyuo Vikuu kama Injini za Ubunifu,” vyuo vinawekewa mikakati ya kuimarisha mifumo, vivutio na ushirikiano utakaorahisisha kuanzishwa kwa biashara bunifu ndani ya taasisi za elimu ya juu. Utekelezaji unafanyika kupitia Mradi wa FUNGUO unaofadhiliwa na Serikali ya Uingereza (FCDO) na kutekelezwa na UNDP Tanzania. Mradi huo unaunganisha wadau wa kitaaluma, wabunifu na watunga sera ili kusukuma mawazo kutoka tafiti hadi kuwa biashara zenye uwezo wa kukua na kuzalisha ajira. Akifungua jukwaa hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mhe. Fatma Mabrouk Khamis, alisisitiza umuhimu wa matokeo halisi ikiwemo tafiti za pamoja, programu za kubadilishana wahadhiri, sera rafiki kwa ubunifu na ujumuishaji wa wanawake na vijana, huku mafanikio yakipimwa kwa idadi ya biashara na ajira zitakazozalishwa. Awamu ya pili ya mpango huo imejikita katika kusaidia makundi ya wanafunzi wenye bunifu zinazotumia teknolojia za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda kama AI, IoT na roboti kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Lengo ni kuzisaidia bunifu hizo kufikia hatua ya bidhaa inayokubalika sokoni (MVP) na hatimaye kuwa biashara kamili katika sekta za nishati safi, kilimo himilivu, miundombinu na uchumi mzunguko.