TheTanzaniaTime

Ubalozi wa Uingereza Waipongeza Tanzania kwa Kukabiliana na Marburg

2026-03-12 - 18:18

Ubalozi wa Uingereza nchini umeipongeza Serikali ya Tanzania kwa mkakati na juhudi kubwa zilizowekwa katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, hususan ugonjwa wa Marburg uliowahi kujitokeza nchini kwa vipindi viwili tofauti. Naibu Kamishna wa Ubalozi huo nchini, Sally Hedley, ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya siku tatu mkoani Kagera, akisema kuwa inafurahisha kuona hatua zilizochukuliwa na mikakati iliyowekwa katika kudhibiti mlipuko huo, ikiwemo ushirikiano uliotokana na msaada na uwezeshaji kutoka kwa wadau wa sekta ya afya. Ameongeza kuwa, kama wadau wa maendeleo katika sekta ya afya, Ubalozi wa Uingereza uliwezesha utoaji wa elimu kwa wananchi pamoja na wahudumu wa afya ngazi ya jamii, hatua ambayo ilisaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti ugonjwa huo. Alisema kutokana na jitihada hizo, Tanzania imekuwa mfano kwa nchi nyingi za Afrika katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko. Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Alex Gasasira, amesema WHO imeendelea kujenga uwezo wa watumishi wa sekta ya afya ili kuimarisha usalama wa kiafya katika maeneo yaliyoathirika. Alieleza kuwa juhudi hizo zimehusisha pia kuboresha maabara, kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa pamoja na kuongeza ushirikishwaji wa jamii katika kudhibiti milipuko. Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maafa na Dharura kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Erasto Silvanus, amesema serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya kukabiliana na dharura za kiafya pamoja na ufuatiliaji wa magonjwa katika jamii, ili kuhakikisha nchi inakuwa salama dhidi ya milipuko ya magonjwa hatari.

Share this post: