TheTanzaniaTime

UAE Yasema Haitakaa Kimya Ikiwa Iran Itaendelea Kushambulia

2026-03-01 - 10:37

Waziri wa Nchi anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa, Reem Al-Hashimy. Falme za Kiarabu (UAE) zimesema hazitakaa kimya endapo Iran itaendelea kurusha makombora na droni dhidi ya nchi hiyo, alisema Waziri wa Nchi anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa, Reem Al-Hashimy, katika mahojiano na CNN. Akizungumza na Becky Anderson wa CNN, Al-Hashimy alisema kuwa UAE iko tayari kujilinda iwapo italazimika, na kusisitiza kwamba nchi hiyo haitakubali kuendelea kuwa mlengwa wa mashambulizi bila kuchukua hatua za kujilinda. Alipoulizwa kama UAE inaweza kubadilisha msimamo wake na kuchukua hatua kali zaidi kijeshi, waziri huyo alisema kuwa hilo linaweza kutokea iwapo mazingira yatalazimu, na kuongeza kuwa sasa uamuzi uko mikononi mwa Iran kuhusu jinsi inavyotaka kushughulika na jirani yake. Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya UAE, Iran ilirusha makombora ya ballistiki 137 na droni 209 kuelekea UAE usiku wa Jumamosi. Wengi wa mashambulizi hayo yalidunguliwa, lakini droni 14 ziliweza kufanikisha malengo yake. Mashambulizi hayo yalilenga miji mikuu ya Abu Dhabi na Dubai, miongoni mwa kitovu cha uchumi na utalii cha nchi hiyo, na kuibua taharuki kubwa miongoni mwa wananchi na wakazi wa kigeni.

Share this post: