TheTanzaniaTime

Tundu Lissu Apinga Ushahidi Mpya Katika Kesi ya Uhaini

2026-02-23 - 14:38

Malumbano makali ya hoja yameibuka mahakamani katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kufuatia hatua ya Jamhuri kuwasilisha notisi ya kuongeza ushahidi mpya. Leo, Jumatatu Februari 23, 2026, upande wa mashtaka umeieleza Mahakama kuwa Februari 18, 2026 uliwasilisha kwa njia ya mtandao notisi ya kuongeza ushahidi katika kesi hiyo. Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, amesema notisi hiyo imewasilishwa kwa mujibu wa kifungu cha 308(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Marejeo ya mwaka 2023. Amesema Jamhuri haiombi kuongeza shahidi mpya, bali inaomba kuongeza ushahidi mpya katika ushahidi wa shahidi wao, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Amin Mahamba, na kwamba kiini cha ushahidi huo kimeambatanishwa. Hata hivyo, Lissu amepinga vikali hatua hiyo, akisisitiza kuwa kifungu cha 308 cha CPA kinahusu shahidi mpya na si ushahidi mpya wa shahidi aliyekwisha kutoa ushahidi. Amesema shahidi mpya ni yule ambaye maelezo yake au ushahidi wake haukuwahi kusomwa katika mwenendo wa awali wa kesi. Aidha, Lissu ametahadharisha kuwa yuko tayari kujadili hadharani yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, akidai kuwa kuingiza ushahidi unaohusiana na mchakato huo kunaweza kufungua mjadala mpana ambao, kwa mujibu wake, dunia inapaswa kuujua. Mahakama inatarajiwa kutoa mwongozo au uamuzi kuhusu uhalali wa notisi hiyo ya kuongeza ushahidi mpya katika hatua zijazo za kesi hiyo inayovuta hisia za wengi nchini.

Share this post: