TheTanzaniaTime

Trump: Mapambano Ya Ardhini na Iran ni Kupoteza Muda

2026-03-06 - 10:07

Donald Trump amepuuzilia mbali uwezekano wa kuanzisha uvamizi wa kijeshi wa ardhini nchini Iran kwa sasa, akueleza mpango huo kama “kupoteza muda” kutokana na kushindwa kwa nguvu za kijeshi za nchi hiyo, ikiwemo Iranian Navy. Akizungumza kwa njia ya simu na NBC News jana Alhamisi, Machi 5, 2026, Trump alijibu vitisho vya hivi karibuni vya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, aliyedai kuwa Iran “inawasubiri” wanajeshi wa Marekani ardhini. Trump alieleza kauli hiyo kuwa “imepotea” na kusema: “Ni kupoteza muda (uvamizi wa ardhini). Wameshapoteza kila kitu. Wamepoteza jeshi lao la majini; wamepoteza kila kitu wanachoweza kupoteza.” Rais Trump aliongeza kuwa kasi na ukali wa mashambulizi ya anga yataendelea hadi mfumo mzima wa utawala wa Iran ubadilike. Ingawa amekataa kuanzisha uvamizi wa nchi kavu, Trump ameweka wazi kuwa lengo lake la mwisho ni kubadilisha utawala wa Iran kabisa. Amesema anataka “kusafisha kila kitu” ili kuzuia mabaki ya uongozi wa sasa kurekebisha mfumo wa zamani ndani ya muongo mmoja ujao. Trump pia alifichua kuwa tayari ana orodha ya watu anaodhani wanaweza kuwa viongozi wema kwa ajili ya Iran baada ya vita. Ingawa hakutaja majina yao, amedai kuwa Marekani inachukua hatua za siri kuhakikisha watu hao waliopo kwenye orodha yake wanabaki hai katikati ya mashambulizi yanayoendelea. Kwa kejeli, Trump alikumbusha kauli yake ya awali kwamba wakati fulani, Waajemi wenyewe watamwita kumuuliza ni nani angetaka awaongoze. “Sijui (nani ataoongoza), lakini wakati fulani watakuwa wananipigia simu kuniuliza ni nani ningependa,” alisema Trump, akibainisha kuwa operesheni za kijeshi haziwezi kuacha nafasi ya mazungumzo na utawala uliopo kwa sasa. Tukio hili linaongeza mvutano mkubwa katika Mashariki ya Kati huku dunia ikifuatilia kwa karibu hatua zinazofuata za Marekani na Iran.

Share this post: