Trump: Iran Inatengeneza Makombora Ya Kushambulia Marekani Hataruhusu
2026-02-25 - 15:28
Rais wa Marekani, Donald Trump Rais wa Marekani, Donald Trump, amewasilisha kwa ufupi hoja yake kuhusu uwezekano wa kushambulia Iran katika hotuba yake ya Hali ya Taifa kwa Bunge la Marekani siku ya Jumanne. Trump amesema Iran inatengeneza makombora yanayoweza hata kushambulia Marekani lakini hataruhusu Iran akiitaja kama mfadhili mkubwa zaidi wa ugaidi duniani kumiliki silaha ya nyuklia. Katika hotuba yake, Trump alielekeza lawama kwa matendo ya Iran ikiwemo kuunga mkono makundi yenye misimamo mikali, mauaji ya waandamanaji, pamoja na programu za nchi hiyo za makombora na nyuklia kama vitisho kwa eneo hilo na kwa Marekani. Madai ya Trump dhidi ya Tehran yanajiri wakati amerundika zana za kivita na jeshi kubwa huko Mashariki ya Kati karibu na Iran. Lakini hapo awali hakuwa ametoa maelezo mengi kuwaeleza wananchi wa Marekani kwa nini anaweza kuanzisha vita kali na Jamhuri hiyo ya Kiislamu. Kwenye hotuba yake ya zaidi ya saa moja na dakika 45 mbele ya mabaraza ya bunge la Marekani, Trump alihoji kuwa, utawala wa Iran na washirika wake wameeneza ugaidi, vifo na chuki. Na kwamba kwa sasa Iran imeanzisha tena programu yake ya nyuklia kwa lengo la kutengeneza makombora ambayo hivi karibuni yatakuwa na uwezo wa kufika Marekani. Rais Trump amewaambia Wamarekani kuwa Warepublican ndio wanaofaa zaidi kuendelea kushughulikia wasiwasi wa umma kuhusu gharama ya maisha. Trump amedai kuwa taifa hilo linahusika na mashambulizi ya mabomu ya kutegwa barabarani ambayo yameua wanajeshi wa Marekani na raia. “Chaguo langu ni kutatua tatizo hili kupitia njia za kidiplomasia. Lakini jambo moja ni hakika: sitaruhusu kamwe mfadhili namba moja wa ugaidi duniani, ambaye bila shaka ndio wao, kumiliki silaha ya nyuklia. Hatuwezi kuruhusu hilo litokee,” amesema Trump.