Trump Atia Saini Amri ya Ushuru Mpya kwa Mataifa Yanayofanya Biashara na Iran
2026-02-08 - 02:29
Washington, Marekani – Rais wa Marekani, Donald Trump, ametia saini amri mpya ya Rais (Executive Order) inayotishia kuyawekea ushuru wa ziada mataifa yote yanayoendelea kufanya biashara na Iran, hatua inayotafsiriwa kama kuongeza shinikizo la kiuchumi dhidi ya taifa hilo la Mashariki ya Kati. Amri hiyo iliyotolewa siku ya Ijumaa, haikubainisha kwa undani viwango kamili vya ushuru vitakavyotozwa, lakini imetaja mfano wa asilimia 25, kiwango ambacho kinaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa biashara kati ya Marekani na nchi zitakazobainika kushirikiana na Iran. Kwa mujibu wa waraka huo, ushuru huo unaweza kutozwa kwa bidhaa zinazotoka Marekani kuelekea mataifa mengine kupitia mfumo wa kuagiza moja kwa moja au njia mbadala za usambazaji. Aidha, amri hiyo imeeleza kuwa kununua, kuingiza au kupata bidhaa kutoka Iran kunaweza kuwa sababu ya nchi au kampuni husika kutozwa ushuru mkubwa zaidi na Marekani. Shinikizo zaidi dhidi ya Iran Ingawa Trump hakulizungumzia moja kwa moja suala hilo wakati wa kutia saini amri hiyo, alisisitiza msimamo wa Marekani kwamba: “Iran haitokubaliwa kamwe kumiliki silaha za kinyuklia,” alisema akiwa safarini ndani ya ndege rasmi ya Rais wa Marekani, Air Force One. Kauli hiyo inaashiria kuendelea kwa sera kali za Washington dhidi ya Tehran, hasa katika masuala ya usalama wa nyuklia. Hatua hiyo inakuja wakati mazungumzo kati ya Marekani na Iran yanaendelea nchini Oman, kufuatia wiki kadhaa za mvutano na vitisho vya kisiasa kutoka pande zote mbili. Mapema mwaka huu, Trump aliwahi kutishia kutoza ushuru wa asilimia 25 kwa mataifa yatakayofanya biashara na Iran kupitia ujumbe aliouchapisha katika mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, akisema: “Kuanzia sasa, taifa lolote ambalo litafanya biashara na Iran litatozwa ushuru wa asilimia 25 kwa biashara zote zinazoshirikisha Marekani.” Hata hivyo, wakati huo hakukuwa na maelezo ya jinsi ushuru huo ungetekelezwa.