TheTanzaniaTime

Trump Adai Iran Yasalimu Amri Kuhusu Nyuklia, Atamba Kupewa Zawadi Kubwa

2026-03-25 - 08:25

Rais wa Marekani, Donald Trump Rais wa Marekani, Donald Trump, amedai kuwa Iran imekubali rasmi kutokuwa na silaha za nyuklia, akisema pia kuwa taifa hilo limetoa “zawadi kubwa sana” kwa Marekani katika mazungumzo yanayoendelea. Trump amesema kwa sasa mazungumzo yanaendelea kati ya Marekani na Tehran, huku akieleza kuwa hatua hiyo ni ishara kuwa pande zote ziko tayari kufikia makubaliano. Akizungumza na waandishi wa habari, Trump alisema: “Iran haitakuwa na silaha za nyuklia hilo ni jambo la kwanza, la pili na la tatu. Wamekubali hilo.” Aidha, alisisitiza kuwa viongozi wa Iran wanataka sana kufikia makubaliano, akieleza kuwa hamu yao ni kubwa kuliko inavyodhaniwa. Katika kauli nyingine yenye utata, Trump alidai kuwa operesheni ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iran imekuwa na mafanikio makubwa, akisema jeshi la Iran limepoteza uwezo wake mkubwa wa kijeshi, ikiwemo anga na majini. Pia alizungumzia mabadiliko ya uongozi nchini Iran, akitaja kuuawa kwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei, na nafasi yake kuchukuliwa na mwanawe, Mojtaba Khamenei, kama sehemu ya kile alichokiita mabadiliko ya utawala. Hata hivyo, Iran imekanusha vikali madai hayo. Spika wa Bunge la Iran, Mohammad-Bagher Ghalibaf, alisema hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika kati ya nchi hiyo na Marekani, akidai taarifa hizo ni propaganda. Wakati huo huo, mvutano umeendelea kuongezeka katika eneo la Strait of Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani. Iran imetishia kulinda eneo hilo kwa nguvu, huku bei ya mafuta duniani ikipanda kwa kasi kutokana na hofu ya usumbufu wa usafirishaji. Ripoti zinaeleza kuwa Marekani inafikiria kupeleka maelfu ya wanajeshi Mashariki ya Kati kuongeza presha dhidi ya Iran, huku Pakistan ikijitolea kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya kidiplomasia. Licha ya kauli za Trump kuonyesha matumaini, wachambuzi wanaona kuwa kufikia makubaliano kutakuwa na changamoto kubwa, hasa kutokana na tofauti juu ya mpango wa nyuklia na makombora ya masafa marefu ya Iran.

Share this post: