TRA Yafungua Kituo Kipya cha Huduma Masaki Kusogeza Kodi Karibu na Wananchi – Video
2026-02-18 - 16:47
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefungua kituo kipya cha huduma katika eneo la Masaki, jijini Dar es Salaam, kilicho chini ya Mkoa wa Kodi Kinondoni, kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi na kurahisisha ulipaji wa kodi. Akizindua kituo hicho Februari 17, 2026, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema hatua hiyo inatokana na Masaki kuwa eneo la kimkakati kibiashara, hivyo kituo hicho kitawawezesha watu wote wanaostahili kulipa kodi katika eneo hilo kutekeleza wajibu wao kwa urahisi. Amesema kufunguliwa kwa kituo hicho ni sehemu ya mkakati wa TRA wa kusogeza huduma karibu na wananchi na kupanua wigo wa kodi, jambo linaloweza kusaidia kupunguza viwango vya kodi siku za usoni iwapo idadi ya walipakodi itaongezeka. Ameongeza kuwa TRA itaendelea kufungua vituo vya huduma za kodi katika maeneo ya kimkakati yenye mzunguko mkubwa wa biashara ili kuwezesha shughuli za kiuchumi, kurahisisha ulipaji wa kodi kwa hiari na kusogeza huduma karibu na wananchi. Aidha, ameiagiza kila mkoa kuhakikisha unakuwa na vituo vya aina hiyo. Kwa upande wake, Meneja wa Mkoa wa Kodi Kinondoni, Azizi Soka, amesema kituo hicho kinatarajiwa kuhudumia zaidi ya walipakodi 6,790 kutoka maeneo ya Masaki, Msasani, Oysterbay, Bonde la Mpunga na maeneo ya jirani, ambapo huduma zote za TRA zitapatikana katika kituo hicho.