TheTanzaniaTime

Tottenham Wamtimua Kocha Thomas Frank Baada ya Matokeo Mabovu

2026-02-12 - 01:39

Thomas Frank Klabu ya Tottenham Hotspur imetangaza rasmi kumfuta kazi kocha wake mkuu, Thomas Frank, kufuatia matokeo mabovu yaliyoikumba timu hiyo katika Ligi Kuu England msimu huu. Uamuzi huo umefikiwa saa chache tu baada ya Spurs kupokea kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Newcastle United katika mchezo wa ligi uliochezwa jana, matokeo yaliyozidisha presha kwa benchi la ufundi pamoja na uongozi wa klabu. Kwa sasa Tottenham wanashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi, wakiwa na tofauti ya pointi tano pekee juu ya eneo la kushuka daraja. Hali hiyo imezua hofu miongoni mwa mashabiki, huku timu hiyo ikiwa imeshinda michezo miwili tu kati ya mechi 17 za ligi msimu huu rekodi ambayo imeonekana kutoridhisha kabisa. Chanzo cha ndani ya klabu kimeeleza kuwa viongozi walilazimika kuchukua hatua ya haraka kujaribu kuinusuru timu hiyo mapema kabla hali haijawa mbaya zaidi. Hatua hiyo inaelezwa kuwa sehemu ya mkakati wa kuleta mabadiliko mapya ya kiufundi ili kurejesha morali ya wachezaji na matokeo chanya uwanjani. Aidha, Tottenham tayari wameanza mchakato wa kutafuta kocha mpya atakayechukua mikoba ya Frank, huku majina kadhaa yakitajwa kuwania nafasi hiyo kwa muda au moja kwa moja. Frank, raia wa Denmark, anaondoka Spurs katika kipindi kigumu huku mashabiki wengi wakitarajia mabadiliko yatakayoiwezesha timu hiyo kurejea kwenye ushindani na kuepuka hatari ya kushuka daraja. Sasa macho na masikio ya mashabiki wa Tottenham yapo kwa uongozi wa klabu kusubiri kutangazwa kwa kocha mpya atakayebeba jukumu zito la kuokoa msimu wao.

Share this post: