TBL Yachukua Hatua Muhimu Kulinda Mifumo ya Maji Jijini Dar es Salaam
2026-03-26 - 16:13
Kampuni ya Tanzania Breweries PLC (TBL) imeadhimisha Siku ya Maji Duniani kwa kuchukua hatua ya moja kwa moja ya kulinda mifumo ya maji jijini Dar es Salaam kupitia zoezi la usafi katika Wilaya ya Ilala. Katika zoezi hilo, zaidi ya wafanyakazi 100 wa kampuni hiyo walishirikiana na viongozi wa jiji pamoja na wadau wa jamii kusafisha eneo la mfereji wa maji taka (effluent discharge channel), ambao una mchango mkubwa katika kulinda mifumo ya maji inayozunguka eneo hilo. Zoezi hilo lilifanyika kwa kushirikiana na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal Juma, viongozi wa Manispaa ya Ilala pamoja na madiwani wa maeneo husika, hatua ambayo inaonyesha ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali katika kulinda afya ya jamii pamoja na mazingira. Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Masuala ya Mawasiliano ya Kampuni hiyo, Neema Temba, amesema maji ni rasilimali muhimu kwa biashara ya kampuni hiyo pamoja na jamii, hivyo kuna wajibu wa kulinda rasilimali hiyo kupitia hatua za vitendo. Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal Juma, amesema ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali za mitaa ni muhimu katika kulinda mazingira ya miji, kuboresha usafi pamoja na kulinda afya ya wananchi. Mbali na zoezi hilo la usafi, TBL imeendelea kushirikiana na Shirika la WWF Tanzania katika miradi ya muda mrefu ya kulinda na kuboresha usalama wa maji, ikiwemo miradi ya miundombinu ya maji inayotumia nishati ya jua katika maeneo kama Kibaha. Aidha, TBL na WWF Tanzania wanaendelea kushirikiana katika kulinda vyanzo vya maji jijini Dar es Salaam, ikiwemo mito ya Msimbazi, Kizinga na Ruvu, ambayo ni muhimu kwa upatikanaji wa maji kwa muda mrefu katika jiji hilo. Kampuni hiyo imeeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi zake za muda mrefu za kulinda mazingira na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali ya maji.