TheTanzaniaTime

Tanzania na Urusi Zakubaliana Kuimarisha Biashara, Nishati na Madini

2026-02-12 - 07:40

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amefanya ziara ya kikazi nchini Urusi tarehe 9 na 10 Februari, 2026 kwa ajili ya kuwasilisha Ujumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Rais wa Shirikisho la Urusi, Vladimir Putin. Wakati wa ziara hiyo, Waziri Kombo amekutana pia kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Shirikisho la Urusi, Mheshimiwa Sergey Lavrov kujadili masuala ya ushirikiano wa uwili kati ya Tanzania na Urusi. Katika mazungumzo hayo pande zote mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati ikiwemo biashara na uwekezaji, elimu, nishati, madini, ulinzi, usalama pamoja na kushirikiana katika ajenda mbalimbali za kimataifa. Aidha, Urusi imeeleza dhamira yake ya kuanza utekelezaji wa Mradi wa Madini ya Urani ujulikanao kama Mkuju River uliopo Namtumbo, Ruvuma utakaotoa fursa ya ajira zaidi ya 4000 kwa Watanzania pamoja na kuzalisha nishati ya umeme wa uhakika, na kuchochea ukuaji wa viwanda Tanzania. Mheshimiwa Waziri Kombo amezungumza na Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Urusi na Mwenyekiti Mwenza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kibiashara na Kiuchumi baina ya Tanzania na Urusi, Maxim Reshetnikov, kuhimiza kasi kwenye utekelezaji maazimio ya vikao vya tume hiyo na kufanya maandalizi ya kina ya kikao cha tatu kinachotarajiwa kufanyika mwezi Mei, 2026 jijini Arusha. Kwa upande mwingine, Kombo amekutana na Waziri wa Uchukuzi wa Urusi, Andrey Nikitin, ambapo pande zote mbili zimekubaliana kushirikiana katika uendelezaji wa Bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, na Bagamoyo, pamoja na katika sekta ya usafiri wa Reli. Serikali ya Urusi itaendelea ku kushirikiana na Tanzania kuifanya kuwa kitovu kikuu cha biashara kwa nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika. Akihitimisha ziara yake, Kombo amezungumza na uongozi wa Shirika la Nguvu za Atomu la Shirikisho la Urusi (ROSATOM), watekelezaji wa mradi wa Urani wa Trilioni 3.06 chini ya kampuni tanzu yake ya Mantara Tanzania Ltd.

Share this post: