TheTanzaniaTime

Sophia Wa Kesi ya Manguruwe Aliyewekeza Mil 14 Akitarajia Kupata Mil 48 Afunguka

2026-01-28 - 14:53

Hii ni updates kutoka mahakama ya hakimu mkazi kisutu inaelezwa kuwa Shahidi ambaye ni Mkulima Sophia Watson (66) ameilezea jinsi alivyotapeliwa Shilingi Milioni 14 baada ya kuwekeza katika Kampuni ya Vanilla International Ltd kwa lengo la kupata Milioni 48 baada ya mwaka mmoja. Sophia ambaye ni Mkazi Njombe ameyaeleza hayo leo katika kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 31523 ya mwaka 2024, Jamhuri dhidi ya Simon Mkondya ‘Manguruwe’ na Rweyemamu Rwezaura ambayo imesikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki. Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Christopher Olembile, shahidi huyo amesema aliifahamu Kampuni hiyo mwaka 2021 kupitia matangazo yaliyorushwa na Kituo kimoja cha television hapa nchini ambapo Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Simon Mkondya, alikuwa akitangaza shughuli za kampuni hiyo inayojishughulisha na kilimo cha mazao mbalimbali ikiwemo vanilla. Amesema baada ya kuona matangazo hayo, alisafiri hadi ofisi za kampuni hiyo zilizokuwa mkoani Njombe ambako alikutana na mfanyakazi aitwaye Gloria Mutabuzi aliyempa maelezo kuhusu zao la vanilla. Aidha, alitembelea mashamba ya kampuni hiyo jambo lililomridhisha na kumfanya kuamua kuwekeza. Shahidi huyo ameieleza Mahakama kuwa Septemba 27, 2021 alilipa jumla ya shilingi milioni 14 kutoka kwenye akaunti yake ya NMB tawi la Njombe kwenda kwenye akaunti ya CRDB ya Vanilla International Ltd. Akiendelea kutoa ushahidi wake ameonesha risiti ya malipo hayo na kuiomba Mahakama ipokee kama kielelezo cha ushahidi, ambapo Mahakama imekubali. Kwa mujibu wa makubaliano, amesema kiasi hicho cha fedha kilipaswa kumuwezesha kumiliki shamba lenye ukubwa wa mita za mraba 300, na baada ya mwaka mmoja angepata faida ya jumla ya shilingi milioni 48. Amedai kuwa baada ya mwezi mmoja tangu kuwekeza, alikwenda kuoneshwa shamba lake na kuliona kabla ya kurejea nyumbani kusubiri muda wa mwaka mmoja uliokubaliwa. Hata hivyo, baada ya mwaka mmoja kukamilika, shahidi amesema alirejea shambani kuangalia maendeleo ya kitalu chake lakini hakuridhishwa na hali ya mazao. Amedai alijaribu kumtafuta Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Simon Mkondya, kwa njia ya simu bila mafanikio, jambo lililomfanya aende katika ofisi za kampuni hiyo Njombe ambako alikuta tayari zilishafungwa. Amesema baadaye alirudi tena shambani na hakukuta mazao yoyote, hali iliyomlazimu kwenda kwa Afisa Kilimo wa eneo hilo kutaka ufafanuzi kuhusu kampuni hiyo, ambapo aliambiwa kuwa alikuwa miongoni mwa watu wengi waliokuwa wakifika ofisini hapo kuulizia sakata hilo. Shahidi huyo ameongeza kuwa baadaye alimuona tena Simon Mkondya kupitia Kituo cha Televisheni akielezea shughuli za kilimo cha vanilla na kudai kuwa ofisi za kampuni hiyo zilikuwa Dar es Salaam katika Jengo la Sky City. Kutokana na hilo, alisafiri hadi Dar es Salaam na alipofika katika ofisi hizo alikutana na Rweyemamu Rwezaura John, mshtakiwa wa pili, ambaye alimueleza kuwa baada ya kushindwa kufanya vizuri Njombe, walihamishia kitalu Zanzibar. Hatimaye, shahidi amesema alifika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe ambapo kupitia Afisa Kilimo, watu wote waliokuwa na madai yanayofanana waliitwa na kuchukua maelezo yao, kabla ya suala hilo kuripotiwa katika Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi za kisheria. Hata hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi January 30, 2026 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Share this post: