Simba Yachapwa Faini ya Milioni 10 kwa Vitendo vya Mashabiki
2026-03-27 - 10:44
Klabu ya Simba imetozwa faini ya shilingi milioni kumi (Tsh. 10,000,000) kufuatia mashabiki wake kuwarushia chupa za maji waamuzi wa mchezo baada ya kumalizika kwa mechi yao iliyomalizika kwa sare ya 1-1 dhidi ya Pamba Jiji FC. Tukio hilo lilitokea katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, wakati waamuzi walipokuwa wakitoka uwanjani baada ya mchezo kumalizika. Hii ni mara ya pili kwa tukio kama hilo kutokea ndani ya kipindi cha miezi miwili, jambo lililochangia kuongezwa kwa uzito wa adhabu hiyo. Uamuzi huo umetolewa Machi 27, 2026 na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Tanzania, kufuatia kikao kilichofanyika Machi 26, 2026, kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa klabu pamoja na kuzingatia kosa la kujirudia. Aidha, tukio la awali lilitokea Februari 25, 2026 ambapo mashabiki wa Simba walimrushia chupa za maji mchezaji wa Dodoma Jiji FC, William Edgar, wakati wa mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Adhabu hiyo inalenga kudhibiti vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyofanywa na mashabiki pamoja na kulinda usalama wa wachezaji, waamuzi na wadau wengine wa soka nchini.