Serikali Yatoa Mwongozo Kwa Waliopoteza Pasipoti Nje ya Nchi – Video
2026-03-26 - 03:34
Ofisa Uchunguzi Mkuu kutoka Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Selestine Makoba. Ofisa Uchunguzi Mkuu kutoka Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Selestine Makoba, amewataka Watanzania walioko nje ya nchi kuhakikisha wanachukua hatua za haraka pindi wanapokumbana na hali ya kunyany’anywa au kupokonywa pasipoti zao. Makoba amesema kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa ajili ya kulinda usalama wa mhusika pamoja na haki zake za msingi, hususan katika mazingira ya ugenini ambako mtu anaweza kukumbwa na changamoto mbalimbali zinazoweza kuhatarisha uhuru wake na ustawi wake. Mtangazaji wa kipindi cha Mapito kinachorushwa na @255globalradio na Global TV, Zaliam Adam akifanya mahojiano na Selestine Makoba . Amefafanua kuwa pasipoti ni nyaraka muhimu inayomtambulisha mtu kama raia wa nchi yake, hivyo kupokonywa kwa hati hiyo kunaweza kumuweka mtu katika hali ya hatari, ikiwemo kushindwa kusafiri au kujieleza rasmi kwa mamlaka husika. Aidha, Makoba amesisitiza umuhimu wa kutoa taarifa mapema kwa ubalozi au ubalozi mdogo wa Tanzania uliopo karibu, pamoja na vyombo vya usalama katika nchi husika, ili kupata msaada na ulinzi stahiki. Ameongeza kuwa Watanzania wanapaswa kuwa waangalifu wanapokuwa nje ya nchi na kuhakikisha wanahifadhi vyema nyaraka zao muhimu, huku wakiepuka mazingira yanayoweza kuwafanya waathirike na vitendo vya udanganyifu au unyanyasaji. Sekretarieti hiyo imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu njia sahihi za kujilinda dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu na vitendo vinavyohusiana na ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kutoa mwongozo wa nini cha kufanya pindi mtu anapokumbana na changamoto akiwa ughaibuni.