Serikali Ya Urusi Yakiri Kuwepo Raia Wao Anayetrendi Kenya Kwa Video Chafu
2026-02-17 - 10:29
Serikali ya Urusi imekiri kuwepo kwa ripoti zinazomhusisha mwanamume mmoja raia wa Urusi anayedaiwa kurekodi matukio ya mapenzi ya wanawake aliokuwa amewarubuni katika nchi mbalimbali za Afrika na kusambaza video hizo mtandaoni bila ridhaa yao, jambo ambalo limezua mshtuko mkubwa na hasira kali katika mataifa ya Afrika na jumuiya ya kimataifa. Ghana imesema wazi kwamba inataka mshukiwa huyo arejeshwe nchini humo ili akabiliwe na mkono wa sheria, ikisisitiza kuwa vitendo hivyo ni uhalifu mkubwa unaokiuka faragha, utu na haki za msingi za wanawake. Mamlaka za Ghana zinasema kuwa tayari zimeanza mchakato wa kisheria na mawasiliano ya kidiplomasia ili kuhakikisha mshukiwa anawajibishwa, lakini zinaeleza kuwa bado hazijapata majibu ya wazi kutoka kwa Moscow kuhusu uwezekano wa kumkabidhi. Katika taarifa fupi, Ubalozi wa Urusi mjini Accra ulithibitisha tu kwamba serikali ya Urusi “inazingatia” madai hayo. Hata hivyo, haikutoa dalili yoyote kama Urusi itakubali ombi la Ghana la kurejeshwa kwa mshukiwa huyo. Wachambuzi wa masuala ya sheria za kimataifa wanasema hatua hiyo inaonekana kuwa ngumu kufikiwa, kwani Urusi mara nyingi huwa haitoi raia wake kwa mataifa ya nje, hasa katika kesi ambazo hazijafikia makubaliano ya makabidhiano ya wahalifu (extradition treaties). Wakati huo huo, Kenya imeanzisha uchunguzi wa mashirika mbalimbali ya usalama na taasisi za haki, ikisema kuwa inashirikiana kwa karibu na washirika wa kimataifa kufuatilia mtandao wa usambazaji wa video hizo na kubaini waathirika waliopo ndani na nje ya nchi hiyo. Serikali ya Kenya imeeleza kuwa kisa hicho ni uhalifu wa kuvuka mipaka unaohitaji kuchukuliwa hatua za haraka, kwa sababu kinahusisha unyanyasaji wa kijinsia, uhalifu wa mtandaoni na uwezekano wa mtandao wa kimataifa wa usambazaji wa maudhui haramu.