TheTanzaniaTime

”Serikali Hailazimishi Transformation Simba, Tutaangalia Katiba” – Msajili

2026-02-18 - 09:17

Msajili wa Vyama vya Michezo na Vilabu nchini, Abel Ngilangwa, amesema Serikali haitaingilia maamuzi ya ndani ya Simba SC kuhusu mchakato wa mabadiliko (transformation) unaoendelea kujadiliwa na wanachama na mashabiki wa klabu hiyo. Akizungumza na waandishi wa habari leo, Ngilangwa amesisitiza kuwa jukumu la Serikali ni kusimamia uzingatiaji wa sheria na katiba za vyama vya michezo, huku akibainisha kuwa maamuzi ya msingi yatabaki kuwa ya wanachama kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa. Amesema mamlaka yake itahakikisha mchakato wowote unaoendelea ndani ya klabu unafuata katiba, kanuni na maslahi ya wadau, hususan mashabiki ambao ni sehemu muhimu ya uhai wa klabu. Kauli hiyo inakuja wakati mjadala mkali ukiendelea mitandaoni kuhusu hatma ya mabadiliko ya uendeshaji wa klabu, huku wadau wakitoa maoni tofauti kuhusu mwelekeo na athari zake kwa mustakabali wa timu. Ngilangwa ametoa wito kwa wanachama na mashabiki kufuata taratibu rasmi za klabu na kuepuka upotoshaji, akisisitiza kuwa utulivu na kuheshimu katiba vitasaidia kufikia maamuzi yenye manufaa kwa klabu na mpira wa miguu nchini kwa ujumla.

Share this post: