Sakata la Ardhi Karagwe: Watoto wa Marehemu Wadai Kudhulumiwa Ekari 32 – Video
2026-01-25 - 21:09
Sakata la familia ya marehemu Cleophace Rutaiga inayoishi Karagwe mkoani Kagera kudai kwamba baba yao mdogo kwa kushirikiana na shangazi yao wamewadhulumu watoto wa marehemu shamba lenye ukubwa wa ekari 32, linazidi kuchukua sura mpya. Global TV imezungumza na mmoja kati ya watoto wa marehemu aliyezungumza kwa niaba ya watoto wengine wa marehemu na kueleza madai hayo ya kudhulumiwa shamba hilo walioachiwa shamba hilo na marehemu baba yao. Global TV pia imezungumza na shangazi anayedaiwa kushirikiana na baba mdogo katika sakata hilo, ambaye ameeleza kuwa madai yanayotolewa na watoto wa marehemu, hayana ukweli kwani hawana nyaraka za kuthibitisha madai yao. Shangazi huyo akaeleza kuwa suala hilo limewahi kupelekwa mahakamani, lakini kesi ikashindwa kuendelea kutokana na walalamikaji kukosa nyaraka muhimu za kuthibitisha madai yao. Global TV pia ilimtafuta baba mdogo anayetajwa kwenye sakata hilo, ambaye naye alikanusha madai hayo. Lakini pia, Global TV ilizungumza na mdogo wa marehemu, ambaye yeye aliwaunga mkono watoto hao na kueleza kuwa ni kweli shamba hilo lilikuwa likimilikiwa na marehemu kaka yao na anawashangaa ndugu hao kwa kutaka kuwadhulumu mali yao.