Rich Mitindo Amzawadia Jackline Wolper Magari Mawili ya Kifahari Valentine
2026-02-14 - 07:40
Mfanyabiashara na mwanamitindo maarufu, Rich Mitindo, amewaacha wengi midomo wazi baada ya kumzawadia mke wake, Jackline Wolper, magari mawili ya kifahari ikiwa ni sehemu ya kusherehekea Siku ya Wapendanao (Valentine). Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Rich alishare video ikionyesha Range Rover Velar ya rangi nyeupe pamoja na Mercedes-Benz C-Class ya rangi nyeusi (AMG Line), zote zikiwa zimefungwa utepe mwekundu kuashiria upendo na mapenzi ya dhati. Akiambatanisha na video hiyo, aliandika: “Wageni wangu wamefika salama, Valentine hii pokea kidogo changu. Inshallah kesho Mungu atatubariki kikubwa zaidi ya hiki. Muhimu ni vile nilivyokupenda tu. Upendo ni vitendo.” Ujumbe huo umeonyesha wazi namna anavyomthamini na kumpenda mke wake, akisisitiza kuwa kwake mapenzi ya kweli hayaishii kwenye maneno bali huonekana kwa matendo. Hatua hiyo imepokelewa kwa furaha kubwa mitandaoni, ambapo mashabiki na watu maarufu mbalimbali wamewapongeza wanandoa hao kwa kuonyesha mfano wa upendo, mshikamano na kuthaminiana ndani ya ndoa.