TheTanzaniaTime

Rais Samia Azindua Soko La Kisasa la Kariakoo (Picha +Video)

2026-02-08 - 12:18

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 08 Februari, 2026, amezindua rasmi Soko la Kisasa la Kariakoo lililopo Jijini Dar es Salaam, hatua inayolenga kuimarisha biashara, usalama na mazingira bora ya kufanyia shughuli za kiuchumi kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla. Akikata utepe kuashiria uzinduzi wa soko hilo, Rais Samia amesema kuwa ujenzi wa soko la kisasa ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya biashara, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa wananchi, hususan wafanyabiashara wadogo na wa kati. Katika hotuba yake wakati wa uzinduzi huo, Rais Samia amewahimiza wafanyabiashara kulitumia soko hilo kwa kuzingatia usafi, nidhamu na ulipaji wa kodi, akisisitiza kuwa maendeleo ya taifa yanategemea ushirikiano kati ya Serikali na wananchi. Soko la Kisasa la Kariakoo linatarajiwa kuwa kitovu muhimu cha biashara Jijini Dar es Salaam, likiwa na miundombinu ya kisasa ikiwemo maeneo ya biashara yaliyopangwa, huduma za usalama, usafi na miundombinu rafiki kwa wafanyabiashara na wateja. Uzinduzi wa soko hilo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wafanyabiashara pamoja na wananchi wa Jiji la Dar es Salaam.

Share this post: