Rais Samia Aomboleza Kifo cha Kardinali Pengo
2026-02-20 - 07:36
Rais Samia Suluhu Hassan ameomboleza kifo cha Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, akieleza kupokea taarifa hiyo kwa masikitiko makubwa. Kupitia salamu zake za rambirambi, Rais Samia amesema katika kipindi chote cha utumishi wake, Kardinali Pengo alisimama imara kuhubiri amani, maadili na mshikamano wa kitaifa, na kwamba alikuwa sauti ya busara katika masuala ya kijamii na kimaadili nchini. Amesema mchango wa kiongozi huyo wa dini katika malezi ya kiroho na maendeleo ya jamii utaendelea kukumbukwa na kuenziwa na vizazi vya sasa na vijavyo. Rais Samia pia ametoa pole kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa, Maaskofu, Mapadri, Watawa, familia ya marehemu, waumini wa Kanisa Katoliki pamoja na Watanzania wote kwa msiba huo. Amehitimisha kwa kumuombea marehemu apumzike kwa amani.