Rais Samia Amshukuru Rais Museveni Kwa Kuunga Mkono Tanzania Kiti cha UN – Video
2026-02-07 - 12:58
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemshukuru Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, kwa uamuzi wake wa kizalendo wa kuiondoa Uganda katika kinyang’anyiro cha kiti cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) ili kuipa nafasi Tanzania. Makubaliano hayo yamefikiwa mkoani Dar es Salaam, siku ya Jumamosi, wakati wa ziara ya Rais Museveni nchini, ikionyesha mshikamano wa nchi hizi mbili katika kusaidiana masuala ya kimataifa. Rais Samia amebainisha kuwa nafasi hiyo ilikuwa zamu ya nchi za Afrika Mashariki, na baada ya mazungumzo ya kidugu, Uganda imekubali kujitoa na kuunga mkono jitihada za Tanzania. Tanzania kwa upande wake imeahidi kuipa nguvu na kuiunga mkono Uganda katika azma yake ya kugombea kiti cha Baraza la Usalama ndani ya Umoja wa Afrika (AU). Aidha, viongozi hao wawili wamejadili hali ya usalama katika Ukanda wa Maziwa Makuu, ambapo Rais Museveni ndiye Mwenyekiti wa nchi za ukanda huo. Rais Samia amethibitisha kuwa Tanzania iko tayari kumuunga mkono Rais Museveni katika mkakati wake wa kuanzisha mazungumzo ya amani ili kurejesha usalama katika maeneo yenye migogoro ndani ya ukanda huo. “Rais Museveni kama mzee wa ukanda, sasa hivi ni Mwenyekiti wa nchi za Maziwa Makuu, na kama mnavyojua ndani ya nchi za Maziwa Makuu usalama hauko vizuri sana. Ana mkakati wa kuanza mazungumzo ya kuleta usalama ndani ya Maziwa Makuu. Nasi Tanzania tumemwambia tunamuunga mkono na tuko tayari kumsaidia atakavyoona inafaa katika jambo hilo,” amesema Rais Samia. Nchi za Maziwa Makuu ya Afrika zinajumuisha Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Nchi hizi ziko karibu na maziwa makuu kama vile Ziwa Viktoria, Tanganyika, Kivu, Edward, na Albert, ambayo ni muhimu kwa maendeleo, usalama, na mshikamano wa kikanda.