TheTanzaniaTime

Rais Samia Afanya Mabadiliko ya Uongozi, Atea Makatibu Wakuu na Wakuu wa Mikoa Wapya

2026-02-07 - 08:08

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mabadiliko kadhaa ya kiutendaji kwa kuwateua viongozi mbalimbali katika nafasi za juu serikalini, yakiwemo uteuzi wa Makatibu Wakuu wa wizara na Wakuu wa Mikoa. Katika uteuzi huo, Balozi Waziri Rajab Salum ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara, akichukua nafasi ya Dkt. Hashil Twaib Abdallah, ambaye atapangiwa majukumu mengine. Ikumbukwe kuwa Balozi Rajab aliteuliwa kuwa Balozi Januari 8, 2026 na kuapishwa Januari 13, 2026, lakini hadi sasa alikuwa hajapangiwa kituo cha ubalozi kabla ya kupewa nafasi hiyo mpya. Makatibu Wakuu wengine walioteuliwa Katika mabadiliko hayo: Dkt. Tausi Mbaga Kida ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Mipango, pamoja na kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango. Dkt. Fred Matola Msemwa ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Uwekezaji. Dkt. James Peter Mataragio ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati (Mafuta na Gesi Asilia). Mhandisi Felchesmi Jossen Mramba ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati (Umeme na Nishati Jadidifu). Wakuu wa Mikoa wapya Kwa upande wa tawala za mikoa: Kanali Yahya Ramadhani Kido ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, akichukua nafasi ya Fatma Mwassa. Kanali Donald William Msengi ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, akimrithi Kanali Patrick Kenan Sawala, ambaye naye atapangiwa majukumu mengine.

Share this post: