Rais Mnangagwa Apendekezewa Mfumo Mpya wa Uchaguzi Kupitia Bunge
2026-02-12 - 01:10
Baraza la Mawaziri la Zimbabwe limeidhinisha rasimu ya sheria inayopendekeza mabadiliko makubwa ya kikatiba, hatua itakayomruhusu Rais Emmerson Mnangagwa (83) kuendelea kusalia madarakani hadi mwaka 2030 au zaidi. Chini ya mapendekezo hayo mapya, mfumo wa kumchagua Rais utabadilika kutoka kura ya moja kwa moja ya wananchi na badala yake Marais watachaguliwa na Wabunge. Aidha, muda wa muhula mmoja utaongezwa kutoka miaka mitano ya sasa hadi miaka saba, huku ukomo ukiwa ni mihula miwili. Licha ya Waziri wa Sheria, Ziyambi Ziyambi, kusisitiza kuwa kutakuwa na mashauriano ya umma kabla ya mswada huo kufika bungeni, wataalamu wa sheria nchini humo wameibua tahadhari. Wataalamu wanahoji kuwa mabadiliko ya ukomo wa muda yanahitaji kura ya maoni ya nchi nzima na si uamuzi wa bunge pekee. Wanasema kisheria, marekebisho ya katiba yanayohusu ukomo wa madaraka kwa kawaida hayapaswi kumnufaisha kiongozi aliyepo madarakani wakati mabadiliko hayo yanapitishwa. Emmerson Mnangagwa, maarufu kama “The Crocodile” (Mamba) kutokana na ujanja wake wa kisiasa, aliingia madarakani mwaka 2017 baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomng’oa Robert Mugabe. Alishinda uchaguzi wa 2018 na 2023, na kwa mujibu wa katiba ya sasa, muhula wake wa mwisho ulipaswa kuishia mwaka 2028. Mabadiliko haya yanakuja miaka 13 tu baada ya Wazimbabwe kupiga kura ya wingi ya Katiba mpya (2013) iliyoweka ukomo wa mihula ili kuzuia kiongozi mmoja kung’ang’ania madaraka, kama ilivyokuwa kwa marehemu Robert Mugabe aliyeitawala nchi hiyo kwa miaka 37. Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV, like, comment ili kuendelea kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika. MJANE ALIYEMWANGUKIA RC CHALAMILA MAPYA YAIBUKA – MMILIKI HALALI HUYU HAPA...