TheTanzaniaTime

Radi Yaua Watu Watatu Wakivuna Mahindi, Mbeya

2026-02-21 - 11:47

Watu watatu wakazi wa Kitongoji cha Goye, Kijiji cha Goye, Kata ya Ndato, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi iliyofuatana na mvua kubwa walipokuwa wamejificha chini ya mti. Kwa mujibu wa taarifa za familia, waliopoteza maisha ni Wilson Sanga (27), Sikuzani Tumaini Sanga (39) na Lucia Joseph Mlumbe (49). Mashuhuda wanasema tukio hilo lilitokea majira ya saa saba mchana Februari 19, 2026, wakati marehemu walipokuwa wakivuna mahindi shambani. Mvua kubwa ilipoanza kunyesha, walikimbilia chini ya mti wa asili kujikinga, ndipo radi ilipowapiga na kusababisha vifo vyao. Mwenyekiti wa Kitongoji alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kijiji, ambaye aliwaarifu polisi. Askari walifika eneo la tukio na kuuchukua miili ya marehemu kisha kuipeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Makandana, Tukuyu kwa uchunguzi zaidi.

Share this post: