Prince Andrew Akamatwa Uingereza Kufuatia Uchunguzi wa Kesi ya Epstein
2026-02-19 - 15:27
Mwana wa familia ya kifalme ya Uingereza, Prince Andrew, amekamatwa na polisi nchini Uingereza kufuatia uchunguzi unaohusishwa na nyaraka zinazojulikana kama Epstein Files. Kwa mujibu wa taarifa za polisi, mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 60 na kitu alikamatwa kwa tuhuma za “utovu wa nidhamu katika ofisi ya umma.” Hata hivyo, mamlaka hazikutaja jina la mtuhumiwa kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa ya utoaji taarifa. Vyombo vya habari vinaripoti kuwa uchunguzi huo unahusiana na madai kwamba mwaka 2010, Andrew alishiriki taarifa za siri za biashara ya Uingereza na mfadhili wa fedha aliyetiwa hatiani kwa makosa ya kingono, Jeffrey Epstein. Wakati huo, Andrew alikuwa akihudumu kama mjumbe maalum wa Uingereza wa masuala ya biashara ya kimataifa nafasi aliyoshikilia kwa takribani muongo mmoja. Polisi walisema wanafanya upekuzi katika anwani mbili tofauti katika maeneo ya Berkshire na Norfolk, mashariki mwa Uingereza. Endapo atapatikana na hatia, kosa hilo linaweza kusababisha apewe adhabu ya kifungo cha muda mrefu kwa mujibu wa sheria za Uingereza. Prince Andrew amekuwa akihusishwa kwa muda mrefu na Jeffrey Epstein, ambaye alikabiliwa na mashtaka ya biashara haramu ya ngono nchini Marekani.