Polisi Wathibitisha Kuachiliwa kwa Andrew Huku Faili za Epstein Zikitajwa
2026-02-20 - 08:17
Andrew Mountbatten-Windsor ameachiwa huru huku uchunguzi ukiendelea kufuatia kukamatwa kwake kwa tuhuma za utovu wa nidhamu katika ofisi ya umma. Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi iliyotolewa Alhamisi jioni, Andrew “ameachiliwa huru huku uchunguzi ukiendelea.” Polisi pia walithibitisha kuwa msako uliokuwa ukiendelea huko Norfolk sasa umekamilika. Kauli hiyo inafuatia kukamatwa kwake mapema, hatua iliyozua mjadala mkubwa ndani na nje ya Uingereza, hasa kutokana na madai yanayohusiana na uhusiano wake na marehemu Jeffrey Epstein. Serikali ya Marekani ilitoa sehemu ya faili zilizokuwa zikihusisha mawasiliano kati ya wawili hao. Akizungumzia suala hilo, Charles III alisema: “Sheria lazima ichukue mkondo wake,” akiongeza kuwa anaunga mkono kazi ya polisi na yuko tayari kutoa ushirikiano wake kamili na wa dhati. Andrew, ambaye awali alijulikana kama Prince Andrew, alipigwa picha akiwa amelala katika kiti cha nyuma cha gari baada ya kutoka kituo cha polisi cha Aylsham, hali iliyoashiria presha kubwa inayomkabili wakati huu wa uchunguzi.