NSSF Yatoa Elimu ya Hifadhi ya Jamii katika Wiki ya Huduma za Fedha
2026-01-27 - 15:03
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) unashiriki katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Usagara, jijini Tanga. Maadhimisho hayo yameandaliwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha ambayo imezialika Wizara za Kisekta ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Ajira na Mahusiano pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo ikiwemo NSSF. Kupitia ushiriki huo, NSSF inaendelea kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi, kuandikisha wanachama wapya pamoja na kuhamasisha wanachama waliopo kutumia mifumo ya kidijitali kupata huduma, ikiwemo mfumo wa NSSF Portal, NSSF App na USSD ( *152*00#). Mifumo hiyo inawawezesha wanachama kupata huduma mbalimbali zikiwemo kupata taarifa za michango yao, kutengeneza kumbukumbu namba za malipo (Control Number), kulipia michango pamoja na kufungua madai ya mafao kwa njia ya mtandao. Aidha, waajiri na wananchi waliojiajiri wameendelea kupewa elimu kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii, kujiunga na NSSF, pamoja na kuhamasishwa kuwasilisha michango yao kwa wakati kwa kutumia mifumo ili kuongeza ufanisi wa hifadhi ya jamii na kuhakikisha wanapata mafao ya muda mfupi na muda mrefu kwa wakati. Katika Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, wananchi wengi kutoka mkoa wa Tanga wamejiunga na NSSF kupitia mpango wa hiari unaoitwa Hifadhi Scheme ambao umeboreshwa na Serikali kwa kutambua umuhimu wa kundi kubwa la wananchi waliojiajiri unaotoa fursa kwa kila Mtanzania kujiunga na NSSF na kufurahia mafao kama wafanyakazi wengine wa nchi hii. Kupitia Hifadhi Skimu (Hifadhi Scheme), mwananchi yeyote anaweza kujiunga kwa kujiandikisha na kuchangia shilingi 30,000 kwa siku, wiki,mwezi au kwa msimu kulingana na kipato chake. Pia, mwanachama atachangia shilingi 52,200 kwa ajili yake na wategemezi wake ambapo watanufaika na pensheni ya uzee, mafao ya matibabu, mafao ya uzazi pamoja na mafao mengine mengi. Wananchi waliojiajiri katika sekta mbalimbali wanaruhusiwa kujiunga na Hifadhi Skimu wakiwemo waliojiajiri katika kilimo, uvuvi, uchimbaji mdogo wa madini, sanaa mbalimbali, bodaboda, bajaji, umachinga, pamoja na biashara ndogo ndogo kama wasusi, wachuuzi wa masokoni, mama/baba lishe, na makundi mengine yanayofanya kazi kwa vipindi maalum. Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yalianza tarehe 19 na yanatarajiwa kufikia kilele tarehe 26 Januari, 2026.