Ndege ya Marekani ya Kujaza Mafuta Yaanguka, Wanajeshi Wafariki
2026-03-13 - 08:17
Picha ya Ndege ya kijeshi ya Marekani ya kujaza mafuta angani aina ya KC-135 Stratotanker Baada ya Kuanguka na Kulipuka Ndege ya kijeshi ya Marekani ya kujaza mafuta angani aina ya KC-135 Stratotanker imeanguka magharibi mwa Iraq wakati ikishiriki operesheni ya kijeshi inayohusishwa na mvutano dhidi ya Iran, huku juhudi za uokoaji zikiendelea. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa asubuhi ya leo Ijumaa Machi 13, 2026 na Kamandi ya Central Command (CENTCOM), imeeleza kuwa ndege hiyo ilikuwa sehemu ya operesheni za jeshi la Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati. Taarifa hiyo imeeleza kuwa ndege mbili zilihusika katika tukio hilo, ambapo moja ilitua salama huku nyingine ikianguka katika eneo la magharibi mwa Iraq. Aidha, haijabainika mara moja kama kuna majeruhi au vifo vilivyotokea kufuatia ajali hiyo. “Tunawaomba watu wawe na subira wakati tunakusanya taarifa zaidi ili kutoa ufafanuzi, hasa kwa familia za wanajeshi waliohusika,” imetahsdharisha kamandi hiyo katika taarifa yake. Ofisa mmoja wa Marekani aliyezungumza na shirika la habari la Associated Press kwa sharti la kutotajwa jina lake amesema ndege iliyoanguka ilikuwa na angalau wahudumu watano ndani. Jeshi la Marekani pia limesisitiza kuwa ajali hiyo haikusababishwa na mashambulizi ya adui wala tukio la kirafiki (friendly fire), likieleza kuwa tukio hilo ni hasara kwa jeshi hilo.