Mwili wa Lukuvi Ulivyowasili Nyumbani Gangilonga Iringa kwa Heshima za Mwisho
2026-03-30 - 09:14
Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), William Lukuvi, umefikishwa nyumbani kwake Kata ya Gangilonga, Manispaa ya Iringa, ukitokea Kiwanja cha Ndege cha Iringa Machi 29, 2026. Mwili huo ulisafirishwa kuelekea Iringa baada ya jana Machi 28, 2026 kuagwa rasmi katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi mbalimbali wa serikali na wananchi walifika kutoa heshima zao za mwisho. Kwa mujibu wa ratiba, mwili wa marehemu Lukuvi utabaki nyumbani kwake Gangilonga hadi Machi 30, 2026, kabla ya kuhamishiwa katika Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Kanisa Kuu la Kihesa, Jimbo Katoliki Iringa kwa ajili ya ibada za kuaga. Baada ya shughuli ya kuaga kukamilika, mwili huo utasafirishwa kuelekea Kijiji cha Idodi kilichopo Iringa Vijijini kwa ajili ya maziko yatakayofanyika Machi 31, 2026. William Lukuvi alifariki dunia tarehe 25 Machi, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu. Shughuli za heshima za mwisho zinaendelea kufanyika kwa utaratibu maalum, huku zikitarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi kutoka maeneo tofauti nchini.