TheTanzaniaTime

Mwigulu Awapongeza Watumishi wa Afya Katavi kwa Huduma Bora

2026-03-16 - 16:58

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema mradi wa ujenzi wa jengo la huduma (Wing B) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi lazima ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa. Akizungumza leo Jumatatu 16 Machi, 2026 baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo katika hospitali hiyo iliyopo Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, Waziri Mkuu amesema Serikali imehakikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. “Matarajio yetu ni kuona mradi unakamilika kwa wakati na kuwa na ubora unaotakiwa. Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya mradi huu, hivyo sitarajii kuona kuna madeni kwa watu waliofanya kazi katika mradi huu,” amesema. Aidha, Waziri Mkuu amewapongeza watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwahudumia wananchi na kuwataka waendelee kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kujituma. “Ninyi mnaofanya kazi nzuri msiingiwe na ubaridi kwa sababu Serikali inaendelea kuwachukulia hatua wale wote wanaobainika kufanya uzembe kazini. Bila ninyi watendaji mnaofanya kazi kwa bidii na weledi, nchi yetu isingekuwa na maendeleo tunayoyaona leo,” amesema. Kadhalika, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye watumishi bora katika sekta ya afya katika ukanda wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), huku akisisitiza kuwa watumishi watakaobainika kufanya uzembe kazini watachukuliwa hatua stahiki. Aidha, Waziri Mkuu amesema kwa takribani miaka 60 baada ya uhuru, wilaya zote za Mkoa wa Katavi hazikuwa na hospitali za wilaya. Amesema mafanikio ya ujenzi wa hospitali mbalimbali yamepatikana katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Share this post: