Mwanamume Ashikiliwa kwa Kumuua Mkewe kwa Kumpiga Kichwani
2026-02-20 - 22:16
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi Kaster Ngonyani. Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi linamshikilia mwanamume mmoja, Busu Lugwisha (51), mkazi wa Kijiji cha Masiko, Wilaya ya Mlele, kwa tuhuma za kumuua mke wake, Regina Thobias (40), kwa kumpiga na kitu butu kichwani. Tukio hilo la kikatili lilitokea usiku wa tarehe 19 Februari, 2026, majira ya saa 04:00 usiku katika Kijiji cha Masigo, Kata ya Ilela, Tarafa ya Inyonga. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Februari 20, 2026, na Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi. Mtuhumiwa, baada ya kuhojiwa na askari, amekiri kuhusika na kifo hicho akidai kuwa alichukua hatua hiyo baada ya mkewe kumnyima tendo la ndoa. “Uchunguzi wa awali na baada ya mtuhumiwa kuhojiwa umebaini chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi kwani mtuhumiwa amekiri kuhusika na tukio hilo na kueleza kuwa amefanya hivyo kwa kuwa mke wake alimnyima tendo la ndoa”, ameeleza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi Kaster Ngonyani. Mwili wa marehemu Regina Thobias umehifadhiwa katika chumba cha maiti katika Kituo cha Afya Inyonga “B” kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu. Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa mara baada ya upelelezi kukamilika, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kukabiliwa na mashtaka ya mauaji. Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limetoa onyo na wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi wanapokutana na changamoto za kifamilia. Badala yake, wameshauriwa kutumia njia za kistaarabu kwa kuwashirikisha viongozi wa familia, viongozi wa dini, wazee wa mitaa, au mamlaka za kisheria ili kupata suluhu ya migogoro yao bila kumwaga damu.