TheTanzaniaTime

Mvutano Mkubwa CUF: Wajumbe Saba Waliyefutwa Wadai Bado Ni Viongozi Halali

2026-02-18 - 16:06

Mvutano unaoendelea ndani ya Chama Cha Wananchi (CUF) sasa umeingia hatua mpya baada ya wajumbe saba wa zamani wa Baraza kuu la uongozi waliokuwa wamefutwa uanachama kurejea na kutangaza kuwa bado ni viongozi halali wa chama hicho. Wajumbe hao walifutwa uanachama kufuatia tuhuma za utovu wa nidhamu, wakidaiwa kuhusika na vurugu zilizotokea tarehe 6 Oktoba 2025 katika ukumbi wa Shaban Mloo, uliopo makao makuu ya chama Buguruni, Dar es Salaam. Tukio hilo liliripotiwa kuhusisha kufungiwa kwa baadhi ya wajumbe ndani ya ukumbi huo na matumizi ya nguvu wakati wa mchakato wa maandalizi ya wagombea wa uchaguzi mkuu wa 2025, hali iliyopelekea Jeshi la Polisi kuingilia kati. Uamuzi wa kuwafukuza ulipitishwa katika kikao cha baraza kuu kilichofanyika Agosti 6, 2025 na kutangazwa hadharani siku iliyofuata na mwenyekiti wa chama, Ibrahim Lipumba. Hata hivyo, wajumbe hao Dauda Hassani, Yasin Ngotwa, Abdallah Dugwa, Faki Mohamed, Rashid Hamad, Mohammed Nassor na Yusuph Mussa sasa wanasema hawatambui uamuzi wa kufukuzwa kwao. Msingi wa hoja yao ni hatua ya ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kutengua uchaguzi uliomweka madarakani Profesa Lipumba na viongozi wenzake watano. Kwa mtazamo wao, ikiwa uongozi uliotoa adhabu dhidi yao umetenguliwa, basi hata maamuzi yake yanapaswa kupoteza uhalali wake kisheria. Kwa mantiki hiyo, wanadai kuwa bado ni wajumbe halali wa baraza kuu na wana haki ya kushiriki shughuli zote za chama hadi pale suala la uongozi litakapopatiwa ufumbuzi wa kikatiba. Kwa sasa, hali ndani ya CUF inaonekana kutawaliwa na taharuki, huku wanachama wakisubiri mwelekeo rasmi wa uongozi au kauli ya mwisho ya kisheria itakayoweza kuhitimisha mvutano huo unaozidi kupanuka.

Share this post: