Mufti Aomboleza Kifo cha Kardinali Pengo Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph – Video
2026-02-23 - 14:08
Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally, leo Februari 23, 2026 amefika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph kwa ajili ya kutoa salamu za pole kufuatia msiba wa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo. Akiwa kanisani hapo, Dkt. Zubeir alieleza masikitiko yake makubwa juu ya kifo cha kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki, akimtaja kuwa alikuwa nguzo muhimu ya maadili, mshauri wa hekima na kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza amani na mshikamano wa kitaifa. Mufti huyo alikumbusha namna Kardinali Pengo alivyokuwa mtu wa kujali na mwenye moyo wa upendo, akitoa mfano wa tukio la wakati wa msiba wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, John Pombe Magufuli, ambapo alimpatia ulinzi maalum (bodyguard) kama ishara ya kujali na kuheshimiana katika kipindi hicho kigumu. Sheikh Dkt. Zubeir amesema tukio hilo linaonesha namna Kardinali Pengo alivyokuwa na roho ya ushirikiano wa kidini na kitaifa, akisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kumkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika kujenga umoja, amani na maadili mema katika jamii.