TheTanzaniaTime

Msajili Atangaza Uchaguzi wa CUF 2024 Batili, Aagiza Urudiwe

2026-02-15 - 03:40

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imetangaza kuwa matokeo ya Uchaguzi wa Viongozi wa Kitaifa wa Chama cha Wananchi (CUF) wa Desemba 2024 ni batili, na imeelekeza chama hicho kurudia mara moja uchaguzi wa nafasi za juu za uongozi. Kupitia barua ya Februari 13, 2026, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alimwandikia Katibu Mkuu wa CUF pamoja na walalamikaji, akiwemo Maftaha Nachuma na Miraji Mtibwiriko, akieleza kuwa uamuzi huo umetokana na uchambuzi wa malalamiko yaliyowasilishwa ofisini kwake. Nafasi Zilizoguswa Msajili amebainisha kuwa chaguzi za: Mwenyekiti wa Taifa (nafasi inayoshikiliwa na Ibrahim Lipumba) Makamu Mwenyekiti Zanzibar Makamu Mwenyekiti Bara zilikikiuka Kanuni ya 7.1.4 ya Kanuni za Uchaguzi za CUF za Mwaka 2018, inayotaka mshindi apate zaidi ya nusu (zaidi ya 50%) ya kura zote halali zilizopigwa. Kwa mujibu wa barua hiyo, hakuna mgombea aliyefikisha kiwango hicho cha kura, lakini walitangazwa washindi, jambo lililokiuka taratibu za chama. Uamuzi huo unaweka presha kwa CUF kuitisha uchaguzi mpya wa nafasi hizo kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa, huku wadau wa siasa wakifuatilia kwa karibu hatua zitakazofuata ndani ya chama hicho.

Share this post: