Mlipuko Mkubwa Watikisa Uwanja wa Ndege wa Dubai Baada ya Drone Kuanguka
2026-03-07 - 12:08
Taharuki kubwa imeripotiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai kufuatia mlipuko mkubwa unaodaiwa kusababishwa na drone ya kujitoa mhanga inayodaiwa kutoka Iran. Tukio hilo limetokea leo Jumamosi karibu na maeneo ya vituo vya abiria katika uwanja huo wenye shughuli nyingi zaidi katika jiji la Dubai. Kwa mujibu wa mashuhuda, mlipuko huo ulisababisha taharuki kubwa katika uwanja huo wa ndege, ambapo abiria walionekana wakikimbia kutafuta usalama huku baadhi ya maeneo ya uwanja huo yakianza kuhamishwa watu haraka. Mamlaka za usalama zilichukua hatua za haraka kwa kusitisha safari za ndege kwa muda na kuanza operesheni za dharura wakati uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo halisi cha tukio hilo. Hadi sasa, mamlaka hazijatoa taarifa rasmi kuhusu idadi ya watu waliojeruhiwa au kiwango cha uharibifu uliosababishwa na mlipuko huo. Uchunguzi unaendelea ili kubaini iwapo drone hiyo ilihusishwa na shambulio la makusudi au tukio jingine la kiusalama.