Mfanyabiashara Aliyepotea Arusha Apatikana Akiwa Amefariki Kondoa – Video
2026-02-19 - 12:36
Saa chache baada ya kuripotiwa kupotea kwa mfanyabiashara wa madini, Abdillah Mussa maarufu kama Banjo, mkazi wa Sanawari jijini Arusha, mwili wake umepatikana katika eneo la Bereko, wilayani Kondoa mkoani Dodoma. Taarifa za awali zinaeleza kuwa mwili huo ulikutwa kandokando ya barabara ukiwa katika hali ya kuharibika, hali iliyoibua taharuki kubwa na maswali kuhusu mazingira ya kifo chake. Akizungumza kwa masikitiko, mtoto wa marehemu, Mussa Abdillah, amesema familia ilipokea simu ikiarifiwa kuhusu kuokotwa kwa mwili katika eneo la Bereko. Baada ya kufika na kufanya utambuzi, walithibitisha kuwa ni wa baba yao. Ameeleza kuwa mwili huo ulikuwa na majeraha makubwa, yakiwemo macho kutobolewa pamoja na mkono kuvunjwa. Kwa mujibu wa familia, Februari 12 mwaka huu marehemu aliondoka nyumbani kuelekea kufanya mazoezi katika jengo la Ngorongoro, kama ilivyokuwa kawaida yake. Hata hivyo, baadaye taarifa zilianza kusambaa kuwa alichukuliwa na watu wasiojulikana, na tangu hapo hakuwahi kuonekana tena hadi mwili wake ulipopatikana Kondoa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limethibitisha tukio hilo na kusema litaendelea kutoa taarifa rasmi mara baada ya kukamilika kwa taratibu za awali za uchunguzi, likieleza kuwa Kamanda wa Polisi yuko kwenye majukumu ya kikazi kwa sasa. Tutaendelea kuwajuza wasomaji wetu kadri taarifa zaidi zitakavyopatikana.