Meli Ya Kijeshi Ya Iran Yazama Ikiwa Na Watu Zaidi Ya 100
2026-03-04 - 13:27
WJeshi la wanamaji na jeshi la anga la Sri Lanka limetumwa haraka kuwaokoa mabaharia wa Iran baada ya meli yao kutuma ishara ya dharura alfajiri na kuanza kuzama karibu na pwani ya kisiwa hicho, mamlaka za Sri Lanka zimethibitisha. Tukio hilo limeibua taharuki kubwa katika ukanda huo wa Bahari ya Hindi huku operesheni ya uokoaji ikiendelea chini ya uangalizi mkali wa serikali. Waziri wa Mambo ya Nje wa Sri Lanka, Vijitha Herath, aliliambia Bunge kuwa ishara ya hatari ilipokelewa mapema asubuhi kutoka kwa meli ya Iran iliyotambulika kwa jina la IRIS Dena. Kwa mujibu wa taarifa hizo, meli hiyo ilikuwa na takribani watu 180 ndani yake wakati ilipoanza kupata matatizo baharini na baadaye kuripotiwa kuzama kwa sehemu. Mara tu baada ya kupokea taarifa hiyo, Jeshi la Wanamaji la Sri Lanka lilituma meli za doria na vikosi maalum vya uokoaji, huku Jeshi la Anga likipeleka helikopta kwa ajili ya kusaidia kuwatafuta manusura na kutoa msaada wa haraka. Operesheni hiyo imefanyika katika eneo la kusini mwa Sri Lanka karibu na bandari ya Galle, ambako pia majeruhi walipelekwa kwa matibabu. Herath amesema mabaharia 30 waliojeruhiwa wameokolewa na kusafirishwa hadi hospitali katika bandari ya Galle kwa ajili ya kupatiwa huduma za matibabu. Baadhi yao waliripotiwa kuwa na majeraha makubwa, huku wengine wakipata matatizo yanayohusiana na kukaa majini kwa muda mrefu. Hata hivyo, hali kamili ya manusura hao bado haijawekwa wazi rasmi.